RSS

Tag Archives: Kenya

Balqis Chelang’at Chepkwony

————————————————————————————————————————————————————-

***** Ifuatayo ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho “Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Kinunue kwa Tshs 17000 na Kshs 900. Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” *****

————————————————————————————————————————————————————-

“Nilipatwa na ugumu kweli kuamini kuwa Yesu hakufa msalabani”

~ Maneno ya Balqis baada ya kusoma kitabu cha Ahmed Deedat (kiitwacho Crucifixion or Cruci-fiction [Ni Kweli Yesu Kasulubiwa au ni Ubunifu tu!])

Hakukuwa na kikomo kwa Caroline Chelang’at Chepkwony, alikuwa mwanafunzi mwenye juhudi sana na siku zote alikuwa akishika nafasi ya juu katika maisha yake ya shule ya msingi. Baba yake alitaka awe daktari lakini mzungu mmoja, rafiki wa baba yake alishauri Caroline awe mtakwimu bima (Actuary). Wakafata ushauri ule. Ni wanafunzi wafanyao vizuri tu kitaifa ndio wanaoweza kupata nafasi katika shule chache za serikali, Kenya na Caroline Chelang’at alikuwa mmoja wa walioteuliwa. Alichagua Shule ya Sekondati ya Alliance (Alliance Girls High School). Shule inayotambulika kwa kutoa elimu nzuri na kufaulisha watoto sana inayotawala vichwa vya vyombo vya habari katika redio, televisheni na magazeti ifikapo kipindi hiko. Wanafunzi wa hapo wanapenda kuiita shule yao kama “bush (kichaka)’ na wanafunzi kama ‘busherians (wanakichaka)’. Jina hilo lisilo rasmi limetokana na msitu mkubwa uliozunguuka shule. Na wala jina hilo halihusiani na rais mstaafu wa Marekani aliyekoswa na kiatu. Shule hiyo mara kwa mara imekuwa ikifanya vyema katika mitihani ya taifa kidato cha nne, ikiwa ni kawaida kuingia kumi bora katika shule za Kenya.

Baada ya kufanya vizuri katika mitihani hiyo ya elimu ya sekondari  ambapo alipata wastani wa A- kwa masomo yote akipata daraja la juu  (A) katika somo la Hisabati, Fizikia, Kemia, Komyuta na Jiografia, Caroline moja kwa moja aliweza jinyakulia nafasi katika vyuo vya elimu ya juu vya serikali. Chuo kikuu cha Nairobi (UoN), chuo kikubwa zaidi Kenya, kilimchukua na chini ya kitivu cha Hisabati akisomea Utakwimu Bima (Actuarial Science). Na Chuo Kikuu hicho cha Nairobi ndiyo chuo pekee Kenya nzima, kwa wakati huo, kitowacho shahada ya Utakwimu Bima. Mwaka huo 2002, Chuo cha Nairobi kilikuwa kikichukua wanafunzi 16 tu Kenya nzima waliochaguliwa na serikali na Chelang’at alikuwa mmoja wa waliostahili.

Akiwa mwaka wa pili wa masomo, Caroline alikutana na Salim, mwanafunzi katika hiko chuo kikuu aliyekuwa akichukua masomo yake katika Kitivo cha Fani (Faculty of Arts). Moja ya vipaumbele vya Salim katika maongezi ilikuwa ni mazungumzo ya dini. Alimchokoza Chelang’at kuhusu imani yake ya dini. Salim alimuomba Chelang’at afanye ufatiliaji mzuri kuhusu dini na yeye akamsikiliza. Bila kupoteza muda, Salim alimkabidhi Chelang’at baadhi ya vitabu na makala yanayoongelea linganishi ya dini mbalimbali, na kumtajia orodha ya tovuti ambazo zinachambua masuala ya dini vyema tena kwa kutumia akili ya kawaida.

Baadhi ya vitabu ambavyo Caroline alivisoma vya Ahmed Deedat ni:

►Is the Bible the Word of God? (Je Biblia ni Neno la Mungu?

►Crucifixion or Cruci-fiction! (Kusulubiwa Kweli au Kusulubiwa kwa Kubuniwa?)

►Resurrection or Resuscitation? (Kufufuka au Kurudishiwa Fahamu?)

►What Was the Sign of Jonah? (Ipi ilikuwa Muujiza wa Yunus?)

►Who Moved the Stone? (Nani Aliyesogeza Jiwe?)

►Qur’an Miracle of Miracles (Qur’an ni Muujiza wa Miujiza)

►What the Bible Says About Muhammad (pbuh)? (Biblia Inasema Nini Kuhusu Muhammad?)

►Christ in Islam (Kristo Ndani ya Uislamu)

►Combat Kit (Zana za Mapigano)

Vitabu hivyo na venginevyo vya Ahmed Deedat vilivunja kabisa imani ya Kikristo ya Caroline na hatimaye alibaki na moja tu la kufanya, nalo ni kuingia katika Uislamu. Hiyo ilikuwa mnamo tarehe 14 Aprili 2005 akiwa na miaka 22 ndipo Caroline alipoamua rasmi kuwa Muislamu na kuliacha jinale la Kikristo na kuchukua la kiislamu akibakisha majina yake ya Kikalenjin (Kalenjin ni moja ya kabila za Kenya). Sasa amekuwa akiitwa Balqis Chelang’at Chepkwony. Kabla ya kusilimu, akili yake ilijaa mawazo mgando na hasi kuhusu Uislamu na Waislamu. “Nilikuwa nikiwachukulia Waislamu kama watu wa ajabu na waliopotea kweli kwani walikuwa wakimuamini Mtume ambaye amekufa,” Alisema. Vitabu vyengine alivyosoma kabla ya kusilimu ni Let the Bible Speak (Wacha Biblia Izungumze) cha Abdul Rahman Dimishkiah, Oneness of God: The Ultimate Solution to the Trinitarian Controversy (Umoja wa Mungu: Suluhisho Thabiti ya Ubishani wa Utatu) cha Marmarinta Umar P. Mababaya na Pillars of Faith (Nguzo za Imani) cha Jaafar Shaikh Idris. Sanjari na hayo, Balqis baada ya kusilimu ameangalia video za Ahmed Deedat akifanya midahalo na wanateolojia mashuhuri wa Kikristo. Dah! Ilimchukua mwezi mmoja na nusu tu, kuhifadhi juzuu Amma, juzuu ya mwisho katika Qur’an iliyo kwa lugha ya Kiarabu (Qur’an ina juzuu 30, Juzuu moja ikiwa na kurasa 20 na Qur’an nzima ina kurasa 604). Japo alibanwa sana na ratiba za masomo shuleni na projects (miradi ya majaribio) bado alithubutu kuhifadhi juzuu nzima ya mwisho ya Qur’an. Hii inaweza kuwa sawa na kuiweka kichwani injili ya Mathayo, neno kwa neno! Msikiti mkubwa zaidi Kenya, Jamia Mosque una kitengo maalumu kwa ajili ya wanaosilimu kikiwa mahususi kuandaa madarasa ya kuwasaidia waliongia katika Uislamu kuijua dini yao. Naye Balqis baada tu ya kusilimu, aliweza kufika hapo, alisoma na kuhitimu masomo hapo katika Taasisi hiyo ya Jamia.

Balqis alifatilia masomo ya Kiislamu kwa dhati, akiendana na aya, “…Kishike Kitabu [yaani dini] kwa nguvu!…” [Q 19:12]. Baada ya kupata shahada yake ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 2006, na kama ilivyo ada kwa mhitimu yeyote, Balqis naye aliingia katika michakato ya kutafuta kazi. Familia na rafiki zake walimsaidia pia katika hilo. Mzazi wake wa kiume, ambaye alikuwa ni mhasibu mkuu (Chief Accountant) wa Chuo Kikuu cha Moi (Moi University),  bila shaka atakuwa anajuana na wafanyabiashara wengi au makampuni mengi. Hii ingetosha kumpatia kazi nzuri yenye hadhi Balqis. Tena kwa shahada aliyokua nayo, alikuwa na asilimia 100 ya kuchukuliwa na mabenki makubwa makubwa au mashirika ya bima.*

Hii lilidhirika ukweli wake pale makampuni mbali mbali yalipoanza kumgombania, wakianzia na kima cha chini cha mshahara cha Kshs 40 000 (takriban 482 $ au Tshs 748,300) kwa mwezi. Ingawa alikuwa hayupo sawa kifedha wakati huo, Balqis alikataa kazi zote hizo kwa sababu kufanya kazi makampuni ya bima na mabenki hayo ya kibiashara yalikuwa ni haram kwa sheria za Kiislamu. “Kha! Atakuwa kashaanza kuwa mwehu!,” Hivyo ndivyo rafiki na ndugu walivyobaki wakisema. Lakini kwa upande wake, ilikuwa ni makosa na kinyume cha maadili (unethical) kufanya kazi katika mashirika yanayoendekeza riba yakipingana na maneno ya Mwenyezi Mungu: “Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba.…”[Q 2:275].

Alikuwa na yakini kuwa akijitenga na kitu kwa ajili ya Allah basi Mwenyezi Mungu atamfidia na kitu kingine bora kuliko alichokiacha. Alifata maneno ya mtume Muhammad kwa nguvu zote: “Huwezi kuacha chochote kwa ajili ya Allah, aliyetukuka, ila atakupa kengine bora badala yake.”[1] Balqis alipozwa moyo na mafundisho ya Uislamu yaliyompa faraja, tumaini na nguvu: “Enyi watu, muogopeni Mola wenu, na muwe na kiasi katika kutafuta maisha ya dunia, kwani hakuna roho itakayoondoka bila kupokea vyote ilivyokadiriwa, hata kama vinachelewa. Hivyo muogopeni Allah na mumche, muwe na kiasi katika kutafuta rizki; chukua lile lililoruhusiwa na uwache lililokatazwa.”[2]

Badala yake, Balqis akaamua kufanya kazi katika kampuni ya ukaguzi wa mahesabu iliyoko huko Nairobi, karibu na barabara iitwayo Mombasa Road. Hapo alikuwa akilipwa Kshs 10,000 (takriban 120 $ au Tshs 187,000) kwa mwezi. Kutoka katika mshahara huo, alitenga Kshs 2500 (takriban 30 $ au Tshs 46,760) kulipia chumba kilicho kama gereza la Guantanamo huko Eastleigh, sehemu iliyopo kiunga cha jiji la Nairobi. Chumba alichokodi kilikuwa na eneo la mita za mraba 2.5 kwa 1.5, kusema kweli ni kidogo sana hata kwa kitanda tu. Alikuwa na godoro tu ambalo alilliegemeza dirishani wakati wa mchana ili ageuze chumba kuwa cha kukaa (sitting room), na kulitandika chini wakati wa usiku  ili afanye sehemu ya kupumzishia ubavu wake (bedroom). Gharama zake za usafiri kuelekea kazini kwake zilikuwa ni Kshs 3 000 (takriban 36 $ au Tshs 37,407) na chakula kilimgharimu Ksh 3 000 kwa mwezi nayo. Ukiachilia mbali gharama nyengine kama matibabu, mshahara wa Balqis haukuwa ukimtosha ila yeye aliendelea kuvumilia.

Baada ya mwezi, akapata kazi nyengine kama msarifu (bursar) wa Shule ya Sekondari ya WAMY (WAMY High School)  akipokea kiasi cha shilingi za Kenya 20 000 (takriban 241 $ au Tshs 374,000). Alifanya kazi hapo kwa miezi miwili kabla ya ahadi ya Mungu kutimia kwake. Alipokea simu asiyoitegemea. “Naongea na Cheleng’at?…,” Mpigaji alihoji, “je unaweza kujipanga kwa ajili ya usaili (interview) wa kazi ofisini kwetu.” Akapata kazi nzuri hapo akiwa mhasibu wa kampuni ya mafuta ya Hass (Hass Petroleum Company) hapo Nairobi. Kampuni hiyo imestawi Afrika Mashariki nzima na maeneno ya maziwa makuu na inazidi kupanua huduma zake sehemu nyenginezo. Balqis anaiita kampuni hii kama baraka kutoka kwa Allah kwani ndio kampuni pekee Kenya inayotenganisha wafanyakazi wake wa kiume na wa kike na inaruhusu wanawake kuvaa mavazi yao ya kidini ikiwemo niqab (kuziba uso). Kampuni pia, imetenga nafasi kwa ajili ya swala na katika nyakati hizo wafanyakazi wanaruhusiwa kusimamisha kazi zao ili waende kuswali. Mshahara wa kuanzia ulikuwa mara dufu ya alichokuwa akipokea katika shule ya WAMY. Sanjari na hilo, kampuni imempa mkopo usio na riba ambao amenuia kuutumia kwa ajili ya kununua mahali pa kuishi Nairobi. Kwa sasa, mshahara wake wa kila mwezi si chini ya Kshs 130 000 (takriban 1,546 $ au Tshs 2,431,510). Sasa anaelewa vizuri zaidi ule usemi wa Mtume kuwa “Huwezi kuacha jambo kwa ajili ya Allah, aliyetukuka ila Yeye atakupa lengine bora badala yake.  Amekana kufanya kazi katika mashirika yanayoenda kwa riba, kwa ajili ya khofu kwa Allah na sasa anafanya kazi katika kampuni yenye mazingira ya kiislamu. Kifupi, dada huyu ana ushujaa wa kumuingiza peponi kwa kumtambua Mungu pale alipokataa biashara haram. Ibn Maood, swahaba wa Mtume na mwanachuoni mkubwa, alitafsiri uchamungu kama ifuatavyo: “….Kumtii Mungu na katu kutomtii Yeye, kumkumbuka Yeye na kamwe kutomsahau, kumshukuru Yeye na kutojaribu kutoonesha shukrani zako kwake.” Na kulingana na msomi mkubwa aitwae Shaykh Muhammad Swaleh al-Uthaymeen, anatoa taarifa ya Ucha Mungu kama: “Al-Muttaqun (Wachaji Mungu) ni wale ambao wanajilinda na adhabu ya Allah kwa kufanya yale aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na kujiepusha na yale aliyoyakataza.”[3]

Kwa sasa, si vibaya kama tukitoka nje ya kisa cha Balqis na kujikumbusha kuwa mahitajio yetu yote yamegawanyika katika vifungu viwili: Ima 1) mazuri ambayo tunayatafuta au 2) mabaya ambayo tunayojiepusha  nayo. Jawabu la mahitajio hayo linapatikana katika aya mbili katika Qur’an. Kama unafanya kazi kuepuka hofu ya magonjwa, kutokua na kazi, mawazo, shida….Mungu anasema: “Na anayemuogopa [anayemcha] Mwenyezi Mungu, (Mwenyezi Mungu) humtengenezea njia ya kuokoka (katika kila balaa).”[ Q 65:2]. Njia ya kutokea kutokana na matatizo yako, mashaka na ugumu unaokupata, hofu ya kufilisika, kutokua na kazi, kuharibu hadhi yako, mabalaa, magonjwa, mgogoro, umasikini, na bila kusahau la muhimu zaidi adhabu kubwa akhera.

Wenye bidii watapata njia ya kufanikisha ndoto zao kwa uwepesi kama wakimtegemea Mungu (sio kumtegea). Vitu unavyotaka kuwa navyo kama kazi nzuri, nyumba nzuri, gari zuri, mke mwema, utajiri na mengineyo yanapatakana kiurahisi iwapo utajiegemeza kwenye uchamungu. Qur’an haikuacha hilo: “Na anayemwogopa [anayemcha] Mwenyezi Mungu, (Mwenyezi Mungu) humfanyia mambo yake kuwa mepesi.”[Q 65:4].  Hata njia yako kuelekea peponi itafanywa rahisi na huu ndio ufanisi mkubwa na wa kweli.

Mafanikio kwa hivyo yanafikiwa kwa daraja ya kumtambua Mwenyezi Mungu na kufuata maamrisho yake. Ndoto zako zote zitatimia kama unamtumaini Yeye kupitia uchamungu wako, na Yeye atakusahilishia njia yako na hofu na mashaka yote yatakuondoka kichwani mwako. Ili kujenga daraja kati ya mafanikio na wewe, uchamungu lazima uzingatiwe. Kuwa mchaMungu kunamaanisha kuitafuta dini ya haki, kujua maamrisho (halal na ya haram) ya Mungu yaliyopo katika maandiko matakatifu ya hiyo dini ya kweli, na kuyafanyia kazi. Kuna ambao wamepata mafanikio bila ya kuwa wachamungu.  Haya “mafanikio” ya kidunia hayatamsaidia akhera. “Mafikio” yao yatakuwa Jahannam (motoni). “Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake?” [Marko 8:36].

Balqis sasa ameolewa, na kwa kuongezea katika hazina yake ya baraka, tarehe 2 Septemba, mwaka wa 2008, Mwenyezi Mungu alimjaalia mtoto (wa kiume). Wakiendeshwa na maneno ya mtu mwenye mafanikio zaidi[4]: “Wapeni jina langu watoto zenu…”[5] wanandoa hao walifurahi kumpa mtoto wao jina la Muhammad. Wakipata mtoto mwengine wakiume wana niya ya kumwita Ahmad.* Jina jengine la Mtume lililotajwa na hata Yesu:

“Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri!” [Q 61:6]

“Vuta pumzi kidogo,” Mtu anaweza kuuliza, “Kweli Yesu alimtabiri ‘Roho mtakatifu’ au huyo mnaemwita Ahmad?” Jawabu litategemea na vipi tuna uhakika na maneno ya Biblia.

Kama kiliandikwa kama wahyi (maneno yaliyokuwa yakimshukia Yesu) au yaliandikwa tu na watu wasiokua na uhusiano wowote. Au labda maneno hayo yalihifadhiwa au yalibadilishwa! Kiukweli jibu linapatikana kwa jinsi tulivyoisoma Biblia. Je tunaisoma Biblia kupitia Historical-Critical Approach (njia ya kuhakiki/kukosoa na ya kihistoria) au Devotional-Approach (ile njia ya kishabiki ya kuamini na kukubali kila kitu katika Biblia hata bila kusaili). Ujinga ulioje kwa mtu ambaye hajasoma hata kitabu kimoja cha kisomi kinachotoa ushahidi kuwa Biblia haifai kuitwa neno la Mungu na yeye aendelee kupayuka kwa ubishi na kusema Biblia itaendelea kuwa neno la kweli la Mungu. Dkt. Lawrence B. Brown ambaye amefanya utafiti mwingi kuhusu usahihi wa maandiko ya biblia ni mmoja wa watu anayepaswa kusikilizwa kwa kusema kauli hii: “Tunajidanganya wenyewe na kualika shutuma na dhihaka kama bado tukiendelea kuamini kuwa Agano La Kale au Jipya ni maandiko yasiyochafuliwa ya Mungu.[6]  Kabla ya kutia shaka swala hilo au kukwepa maneno ya msingi ningeshauri, jawabu lolote la kisomi la kujibu kauli ya Dkt Brown, lingetangulizwa na kusoma kitabu chake chochote kama Mis’Goded au kazi nyengine yoyote inayoleta shutuma hizo kwa Biblia kama kitabu Misquoting Jesus: The Story Behind Who Changed the Bible and Why? (Kumnukuu Vibaya Yesu: Kisa Kinachozungumzia Aliyebadilisha Maandiko ya Biblia na Kwanini Alifanya Hivyo) kilichotungwa na msomi mashuhuri duniani wa Biblia, Bart D. Ehrman. Bart D. Ehrman ni profesa wa Taasisi ya James A. Gray na ni mweneyekiti katika kitivo cha masomo ya dini cha Chuo Kikuu cha North Carolina huko Chapel Hill. Alipokea Tuzo mwaka 1994 ya Philip and Ruth Hettleman (Phillip and Ruth Hettleman Prize for Artistic and Scholarly Achievement) kwa tasnia yake ya sanaa ya uandishi na mafanikio yake. Kwa maelezo zaidi kuhusu Ehrman, tembelea tovuti, http://www.bartdehrman.com. Kutoka katika kitabu cha Jesus Interrupted, Bart D. Ehrman anasema:

“Wasomi wamepiga hatua kubwa kuielewa Biblia kwa miaka mia mbili ilyopita na matokeo ya kusoma kwao yanafunzwa kwetu kila siku, kwa wahitimu wa elimu ya juu na mapadri mbalimbali wanaosomea kuja kufanyia kazi upadri wao. Lakini bado jambo hili limekuwa adimu mno katika vichwa vya wengi. Na matokeo yake, sio tu Wamarekani wengi wanazidi kuwa ‘vihio’ (wajinga) kwa yale yaliyoandikwa katika Biblia, lakini pia wako kizani, hawana  utambuzi wa yale ambayo wasomi waliyasema na waliyoyagundua kwa karne hizi mbili zilizopita.[7]

 

Kauli nyengine itakayotuma mawimbi makali ya hofu ni ya yule Profesa John Rogerson wa Chuo Kikuu cha Sheffield, iliyochapishwa na  The Expository Times, jarida la muda mrefu la masomo ya Biblia, na uchungaji. Inasema kwamba “Majumuiko mengi [ya Wakristo] wanawekwa kizani na huwa  hawafahamishwi zile gunduzi za ubatili wa maandiko ya Biblia [zinazogunduliwa na wasomi wa Biblia].”[8]

Tukizungumzia aya ya Qur’an inayothibitisha utabiri wa Injil kuhusu kuja kwa Muhammad, ni vyema tukajifunza kuwa ndani ya Biblia, kuna neno Paraclete (kutoka katika lugha ya Kigiriki parakletos) lenye maana ya ‘Msaidizi’. Inaweza ikawa bahati tu au imepangwa kuwa hivyo kuwa neno Paraclete limetokea mara tano tu katika Biblia, na mara zote tano limesemwa na Mt. Yohana: Waraka (Barua) ya kwanza yohana 2:1; na Yohana 14:16, 14:26, 15:26, 16:7.”[9] Uchunguzi wa kina unaotuacha tukipigwa na butwaa unatuonesha kuwa hata katika Qur’an, Mtume ametajwa kwa jina mara tano tu (Q 3:144; Q 33:40; Q 47:2; Q 48:29 na Q 61:6). Basi tusitafakari?!!

Balqis sio mpenzi pekee wa Muhammad, Mtume wa Mungu. Gazeti la The Times linaripoti kuwa “Muhammad kwa sasa ni jina la pili maarufu baada ya Jack kwa kupewa watoto wa kiume Uingereza na linatazamiwa kushika namba moja ifikapo mwanzoni mwa mwaka kesho, uchunguzi wa The Times umegundua.”[10] Na Januari 2005, makala ya The Guardian ilisema kwamba: “Huko Brussels, Mohammed limekuwa jina maarufu zaidi kwa watoto wote wanaozaliwa kwa miaka minne iliyopita.”[11] Pamoja na hilo, katika kitabu Religion on the Rise, Hofmann anasema: “…kwa miaka kadhaa sasa, ‘Muhammad’ limekuwa jina linalopewa kwa watoto wengi Ufaransa.”[12]

Tukirejea katika kisa cha Balqis. Nilisahau kusema kuwa Balqis amesomea Kifaransa, Alliance Francaise hapo Nairobi. Balqis alisoma Kifaransa kupitia  Alliance Française, Nairobi. Vile vile, anayo shahada ya CPA (K), ambayo inapatikana kwa kufaulu sehemu sita zote za mitihani hiyo ya wahasibu wataalamu iliyo  chini ya usimamizi wa Bodi ya Wahasibu Wataalamu wa Kenya na Sekretarieti za Mitihani ya Taifa (Kenya Accountants and Secretaries National Examination Board, KASNEB). Pamoja na kusoma masomo ya dini ya Kiislamu amekuwa akijituma kujifunza Kiarabu anapokuwa peke yake. Na ameendelea kwa hilo kwani sasa ameweza kuthubutu kusema, “Hakuna anayeweza kunisema kwa kiarabu nikiwa hapo hapo.”

Tarehe 30 Januari 2010, Nairobi, alizaliwa mtoto mwingine. Balqis alibarikiwa kuwa na mtoto wa pili na siku 7 baada ya kujifungua, mtoto akaitwa rasmi jina la Ahmad. Balqis Chelangat kwa sasa ameshakuwa mama wa watoto wawili, Muhammad na Ahmad.

Njia ya Mawasiliano:

P.O. Box 102489 – 00101

Nairobi,

Kenya.

Barua pepe: balqischepkwony@yahoo.com

simu: +254722941896

REJEA


[1]. Ahmad # 22565. Imethibitishwa kuwa swahih na Albaaani katika al-Silsilah al-Da’eefah, hadith na.5

* Tazama katika Fataawa al-Lajnah al-Daa’imah li’l-Buhooth al-‘ILmiyyah wa’l-Ifta’, 15/9: {“Bima ya maisha ni aina ya bima ya biashara, ambayo ni haram, kwani ina kamari, kubahatisha, riba na kuchuma mali kusikofaa. Hairuhusiwi kufanya kazi katika makampuni ya bima, kwa sababu unajumuika kuiendeleza dhambi jambo amablo pia Allah amelikemea, kama asemavyo: “…Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.” [Q 5:2]}

[2]. Ibn Maajah # 2144, imethibishwa kuwa swahiih na Al-albaani katika Saheeh Ibn Maajah.

[3]. Al-Uthaimin, Al-Allamah Muhammad bin Salih. Commentary on Shaykh Al-Islam Ibn Taymiyyah’s Al-Aqidah Al-Wasitiyyah. Riyadh: Darussalam, 2009. Vol. 1. p. 302.

[4]. Dkt. Michael H. Hart aliandika kitabu alichokiita The 100: A Ranking of the Most Influential Persons in History (Orodha ya Watu 100 Mashuhuri Walioacha Athari ya Mafanikio Katika Ulimwengu Huu) na akiwashangaza wengi, aliona ni mtu mmoja tu aliyefaa kushika nafasi ya juu kabisa katika orodha hiyo naye si mwengine bali ni Mtume Muhammad. Tazama Hart, Michael H. The 100: A Ranking of the Most Influential Persons in History. New York: Kensington Publishing Corp., 2000.p.3.

[5]. Muslim Bk. 25, No. 5325. Tazama pia Bukhari Vol. 8, Bk. 73, No. 207; Bukhari Vol. 8, Bk. 73, No. 216; Bukhari Vol. 8, Bk. 73, No. 217.

* Pamoja na hivyo, Mtume alishasikika akisema: “Mimi nina majina mengi, Muhammad, pia naitwa Ahmad, Maahi (aliyefuta) ambaye Allah akafuta ukafiri kupitia yeye. Mimi pia ni Haashir ambaye atafufuliwa mwanzo siku ya Qiyama. Mimi pia ni ‘Aaqib (wa mwisho katika kuja Mitume na pia hakutakuwa na Mtume baada yake).” Angalia Tirmidhi Chapter 51, Hadith No. 1 (360).

[6]. Brown, Laurence B. MisGod’ed: A Roadmap of Guidance and Misguidance in the Abrahamic Religions. USA: BookSurge Publishing, 2007.p. 219.

[7]. Ehrman, D. Bart. Jesus Interrupted. Front Flap. New York: HarperCollins Publishers, 2009. ; Also see “Cover Content From the Publisher.” bartdehrman.com. Retrieved on 25 Nov. 2009. <http://www.bartdehrman.com/books/jesus_interrupted.htm&gt;

[8]. Professor John Rogerson of Sheffield University, in The Expository Times, 113/8, p.255.

[9]. New Catholic Encyclopedia. Vol 10, p. 989.

[10]. Nugent, Helen and Nadia Menuhin. “Muhammad is No 2 in boy’s names.” The Times 6 June 2007.

[11]. Browne, Anthony. “The Triumph of the East.” The Guardian 27 Jan. 2005.

[12]. Hofmann, Murad Wilfried. Religion on The Rise: Islam in the Third Millennium. Maryland: Amana Publications, 2001.p. 183.

Advertisements
 
Leave a comment

Posted by on November 16, 2012 in Waliosilimu

 

Tags: , , , , ,